FDH yatoa wito kwa watu wenye ulemavu kujilinda dhidi ya El Niño

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Shirika la Foundation for Disabilities Hope (FDH) limewataka watu wenye ulemavu kuchukua tahadhari na hatua za mapema kujilinda dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño, huku likitoa wito maalumu wa kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapewa kipaumbele katika maandalizi ya kukabiliana na majanga.


Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa FDH, Maiko Salali, ambaye amesema shirika hilo linaendelea kufuatilia kwa karibu taarifa na utabiri unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu hali ya hewa na madhara yanayoweza kujitokeza.


Salali amesema FDH imekuwa ikishirikiana na Serikali pamoja na mamlaka husika kutoa elimu na tahadhari kwa watu wenye ulemavu, ambao amesema ni miongoni mwa makundi yanayoweza kuathirika zaidi wakati wa majanga kutokana na changamoto zinazohusiana na aina mbalimbali za ulemavu.


Amesema ni muhimu taarifa za tahadhari kuhusu El Niño na majanga mengine ziwafikie watu wenye ulemavu kwa wakati na kwa namna inayowawezesha kuzifahamu na kuchukua hatua stahiki za kujilinda.


“Tunatakiwa kuchukua hatua kwa kushirikiana na Serikali katika kuwaelimisha na kuwasaidia ndugu zetu watu wenye ulemavu ili waweze kupata elimu na uwezo wa kuchukua hatua za kujikinga dhidi ya majanga haya,” amesema Salali.


Aidha, amewataka wadau mbalimbali, wazazi, walezi na Watanzania kwa ujumla kushirikiana katika kuhakikisha watu wenye ulemavu hawaachwi nyuma katika mipango ya kukabiliana na athari za El Niño.


Salali amesema kutokana na changamoto za ulemavu, baadhi ya watu wenye ulemavu wanaweza kupata ugumu wa kufikia huduma, taarifa na fursa mbalimbali wakati wa majanga, hivyo kuna umuhimu wa programu za tahadhari, uokoaji na msaada kuzingatia mahitaji yao.


Pia amewataka watu wenye ulemavu wenyewe kufuatilia kwa karibu taarifa zinazotolewa na TMA pamoja na vyombo vingine vinavyohusika ili waweze kuchukua hatua kwa haraka pale kunapotolewa tahadhari.


Amesema FDH itaendelea kutoa elimu na kushirikiana na Serikali na mamlaka husika kuhakikisha taarifa muhimu zinawafikia watu wenye ulemavu na kuwawezesha kujiandaa kukabiliana na athari za majanga.


“Tunawaomba Watanzania tushirikiane kulisaidia kundi hili ili liweze kupata uelewa wa kutosha na namna ya kukabiliana na changamoto hizi, ili tujenge jamii ambayo haimuachi mtu nyuma,” amesema Salali.

Post a Comment

Previous Post Next Post