Na Carlos Claudio, Dodoma.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limeweka mkakati wa kuhakikisha watoto na vijana wanashirikishwa kikamilifu katika kutafuta na kutekeleza suluhisho za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yamesemwa leo, Septemba 16, 2026, jijini Dodoma na Mtaalamu Mshauri wa Mabadiliko ya Tabianchi kutoka UNICEF, Dkt. Sixbert Mwanga, wakati akizungumza katika Kongamano la Vijana kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (LCOY Tanzania), lililowakutanisha vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Dkt. Mwanga amesema UNICEF imechukua hatua hiyo kwa kutambua kuwa watoto na vijana siyo waathirika pekee wa mabadiliko ya tabianchi, bali pia ni sehemu muhimu ya suluhisho, wakiwamo kama rasilimali, nguvu kazi, wabunifu na wazalishaji wa mawazo na teknolojia zinazoweza kusaidia kukabiliana na changamoto hizo.
Amesema mpango huo umejikita katika maeneo matatu muhimu, ikiwamo kuhakikisha watoto na vijana wanalindwa dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, kuwawezesha kupata ujuzi na maarifa yanayohitajika, pamoja na kuwafikisha katika majukwaa ya maamuzi ya kitaifa na kimataifa ili waweze kutoa sauti na mchango wao.
Aidha, amesema UNICEF inalenga kuhakikisha shughuli zake haziongezi madhara kwa mazingira na badala yake zinazingatia hatua za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumzia ushiriki wa vijana katika LCOY Tanzania, Tunu Kalanje kutoka Humanitarian Information Knowledge Foundation (HUDEFO), ambaye alikuwa miongoni mwa wajumbe wa kamati ya maandalizi ya kongamano hilo, amesema mkutano huo umetoa nafasi kwa vijana kujadili changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuandaa Tamko la Kitaifa la Vijana kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.
Kalanje amesema vijana wanataka kuona utekelezaji wa sera na mikakati ya mabadiliko ya tabianchi ukiimarishwa, akieleza kuwa Tanzania ina sera nzuri, lakini changamoto imekuwa katika utekelezaji wake.
“Tunatamani kuona utekelezaji wa sera ambazo zinahusiana na mabadiliko ya tabianchi ukizingatiwa zaidi, kwa sababu sisi kama vijana hatuna tatizo la kuwa na sera nzuri. Sera zetu ni nzuri sana, lakini utekelezaji wake ndiyo umekuwa kidogo,” amesema.
Amesema vijana pia wanahitaji fursa zaidi za kushiriki katika mikutano ya kimataifa inayohusu mabadiliko ya tabianchi, huku akitaka nafasi hizo ziwe wazi na rahisi kufikiwa na vijana.
Aidha, Kalanje amesema vijana wanahitaji kuwa na Baraza la Vijana la Mabadiliko ya Tabianchi, litakalowapa nafasi ya kujadili changamoto zinazowakabili na kutoa mapendekezo kwa serikali na wadau wengine.
Kwa upande wake, Agnes Petro kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), amesema ameshiriki kongamano hilo kwa lengo la kujifunza namna vijana wanavyoweza kutumia teknolojia na ubunifu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema vijana wanaweza kutumia teknolojia kuonyesha athari za mabadiliko ya tabianchi katika jamii zao na kutengeneza suluhisho zinazoweza kutumika katika maeneo mbalimbali.
“Kule chuoni kwetu tulitengeneza ramani ya kuonyesha athari zilizotokea kutokana na mafuriko. Nimekuja na uzoefu huo kwa vijana wenzangu ili tuweze kujadili namna teknolojia inaweza kutumika kuleta mabadiliko katika masuala ya tabianchi,” amesema.
Naye Emmanuel Elisha Sironga, mwanafunzi wa udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma na mshiriki kutoka Save Youth Dreams Foundation, amesema kongamano hilo limempa uelewa zaidi kuhusu nafasi ya vijana katika kutengeneza sera na kushiriki katika maamuzi yanayohusu mabadiliko ya tabianchi.
Sironga amesema moja ya maeneo yaliyomvutia ni mjadala kuhusu matumizi ya akili mnemba (AI) na uhusiano wake na mazingira, hususan matumizi ya nishati na maji katika vituo vya kuhifadhi na kuchakata taarifa, maarufu kama data centres.
Amesema vijana wanahitaji kuendelea kujadili namna teknolojia hiyo inavyoweza kutumika kwa kuzingatia ulinzi wa mazingira.
Wakati huo huo, Hilda Sunday kutoka Agri Youth Forum Dodoma, amesema kongamano hilo limemsaidia kutambua nafasi waliyonayo vijana katika kuchangia hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema wanawake, watoto na vijana ni miongoni mwa makundi yanayokumbwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo wanapaswa kushirikishwa katika kutafuta suluhisho.
Kwa upande wake, Theresia Charles kutoka Tanzania Girl Guide Association, amesema wanawake na wasichana wanapaswa kuwa sehemu ya michakato ya kutunga sera za mabadiliko ya tabianchi kutokana na changamoto wanazokutana nazo zinazohusiana na mabadiliko hayo.
Amesema ushiriki wa wanawake na wasichana katika utungaji wa sera utasaidia kuhakikisha changamoto zinazowakabili zinazingatiwa katika mipango na mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Vijana walioshiriki LCOY Tanzania wameendelea kusisitiza umuhimu wa kushirikishwa katika utengenezaji na utekelezaji wa sera, pamoja na kupata fursa za kushiriki katika majukwaa ya kitaifa na kimataifa yanayojadili mabadiliko ya tabianchi.
Wamesema ushiriki huo utawapa nafasi ya kutumia maarifa, teknolojia, ubunifu na nguvu kazi yao katika kutengeneza suluhisho za changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinazoikabili Tanzania.


Post a Comment