Agri Youth Forum: vijana wapewe nafasi katika teknolojia na ubunifu wa kilimo.



Na Carlos Claudio, Dodoma


Vijana nchini wametakiwa kutumia ipasavyo teknolojia, ubunifu na maarifa katika sekta ya kilimo ili kujenga fursa za ajira, biashara na kuongeza thamani ya mazao.


Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Kilimo, Gungu Mibavu, wakati akizungumza katika Kongamano la Vijana la Kilimo Ikolojia Tanzania 2026.


Mibavu amesema kijana mwenye maarifa anahitaji mazingira yatakayomwezesha kutumia maarifa hayo, huku mwenye bidhaa akihitaji soko na mwenye teknolojia akihitaji nafasi ya kutengeneza na kujaribu suluhisho zinazoweza kujibu changamoto zilizopo katika jamii.


Amesema vijana wanaojihusisha na biashara wanahitaji mazingira wezeshi yatakayowawezesha kukuza shughuli zao na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya uchumi.


Aidha, amesema teknolojia za kidijitali, taarifa za masoko na mifumo mbalimbali ya usimamizi zinaendelea kubadilisha namna watu wanavyofanya biashara na kutafuta fursa, hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha teknolojia hizo zinawafikia vijana na kutumika katika kutatua changamoto halisi.



Mibavu amesisitiza kuwa ni muhimu kujiuliza iwapo teknolojia zinazotengenezwa zinaweza kutatua changamoto zinazowakabili vijana na walengwa wengine, badala ya kubaki katika mipango na kauli zisizotekelezeka.


Amesema vijana wanapaswa kupewa nafasi katika maeneo yenye umuhimu kwa mustakabali wa kilimo na maendeleo ya taifa, huku wakipatiwa maarifa, teknolojia, mitaji na mazingira bora ya kukuza ubunifu na biashara zao.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Agri Youth Forum, Isaya Silungwe, amesema taasisi hiyo inaendelea kuhakikisha vijana wanakuwa sehemu muhimu ya mnyororo wa kilimo ikolojia kwa kuwajengea uelewa na kuwapatia maarifa kuhusu fursa zilizopo katika sekta hiyo.


Silungwe amesema Agri Youth Forum inalenga kuhakikisha vijana wanaelewa sera na mikakati ya serikali inayohusu kilimo ikolojia, ikiwemo mikakati ya kitaifa inayohamasisha uzalishaji wa kilimo endelevu.


Amesema hatua hiyo itawasaidia vijana kutambua fursa zilizopo katika utekelezaji wa mikakati hiyo na kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa kilimo ikolojia.


“Tunatamani kuwafundisha vijana wajue ni fursa zipi zinazopatikana katika mikakati ya serikali katika kuhakikisha kilimo ikolojia kinaendelea,” amesema Silungwe.


Ameongeza kuwa Agri Youth Forum kama mwamvuli wa vijana katika sekta ya kilimo, ina nafasi kubwa ya kuwaunganisha vijana na fursa zilizopo katika mnyororo wa kilimo ikolojia, pamoja na kuwahusisha katika mijadala ya mbegu, sera, teknolojia na maeneo mengine muhimu.



Silungwe ameishukuru Serikali kwa kutambua nafasi ya taasisi za vijana na wadau wa kilimo ikolojia katika kuleta mabadiliko, akisema ushiriki wa vijana ni muhimu katika kujenga mifumo ya uzalishaji inayolinda ardhi, mazingira na usalama wa chakula.


Amesema kongamano hilo la siku tatu linatoa fursa kwa vijana na wadau kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya vijana, usalama wa chakula, uhifadhi wa ardhi na matumizi endelevu ya rasilimali kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

“Tunataka kuhakikisha ardhi yetu inakuwa salama, mazao yanakuwa salama na ulaji unakuwa salama,” amesema.


Aidha, amewashukuru wadau wote walioshiriki kufanikisha kongamano hilo, akisema mijadala na maarifa yatakayopatikana yanapaswa kuwasaidia vijana kuchukua hatua na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.


Amesema Agri Youth Forum inaamini kuwa usalama wa chakula na ulaji bora lazima uanze katika msingi wa uzalishaji, huku kukiwa na haja ya kubadilisha mitazamo kuhusu maendeleo, uzalishaji na ulaji wa vyakula.

Post a Comment

Previous Post Next Post