Na Carlos Claudio, Dodoma
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Mhe. Jabir Shekimweri, amewataka wadau mbalimbali wa maendeleo, ikiwemo sekta binafsi, mashirika na wafanyabiashara, kuendelea kushirikiana na Habitat for Humanity Tanzania katika kuboresha makazi ya wananchi wenye kipato cha chini na familia zenye uhitaji.
Shekimweri ametoa wito huo jijini Dodoma wakati wa hafla ya makabidhiano ya nyumba ya gharama nafuu iliyojengwa na Habitat for Humanity Tanzania katika Kata ya Ng’ong’ona na kukabidhiwa kwa familia ya watoto yatima waliokuwa wakiishi katika mazingira yasiyokuwa salama.
Amesema Serikali inatambua mchango wa mashirika na wadau mbalimbali katika kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata makazi bora na salama.
“Ninawapongeza sana Habitat for Humanity kwa kazi mnayoifanya. Ni muhimu wadau wengine kuendelea kushirikiana nao ili kusaidia familia zenye uhitaji na kuboresha maisha ya wananchi,” amesema Shekimweri.
Amesema Serikali haiwezi kufanya kila jambo peke yake, hivyo ushirikiano na sekta binafsi, mashirika na taasisi nyingine ni muhimu katika kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taifa wa Habitat for Humanity Tanzania, Magdalena George, amesema shirika hilo linaamini kuwa kila mtu anapaswa kuishi katika nyumba bora, salama na yenye mazingira yanayolinda utu na ustawi wa familia.
Amesema ujenzi wa nyumba ni sehemu ya shughuli zinazotekelezwa na shirika hilo, lakini kazi yao inaenda zaidi ya kujenga makazi, kwani pia wanatekeleza miradi ya maji, usafi wa mazingira, vyoo bora pamoja na kuwawezesha wananchi kiuchumi.
George amesema shirika hilo pia hushirikiana kwa karibu na Serikali kuhakikisha wanufaika wa miradi ya nyumba wanapata nyaraka zinazothibitisha umiliki halali wa makazi yao, ili kuwa na uhakika wa umiliki na kulinda mali zao.
Amesema nyumba bora inaweza kuwa kichocheo cha maendeleo ya familia kwa sababu inatoa mazingira salama ambayo yanaweza kusaidia watoto kupata elimu, familia kuwa na usalama na wananchi kuishi kwa heshima.
“Tunajua kujenga nyumba ni jambo kubwa, lakini tunaangalia pia namna ya kuwawezesha wananchi kuboresha nyumba zao. Tunataka kila mtu awe na sehemu salama na bora ya kuishi,” amesema Magdalena.
Ameongeza kuwa Habitat for Humanity Tanzania inaendelea kutafuta fursa za kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia miradi ya uzalishaji na shughuli za kujipatia kipato, ili wanufaika waweze kuendelea kuboresha maisha yao na makazi yao.
Amesema changamoto ya upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu nchini inahitaji ushirikiano mpana kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha, mashirika ya kijamii na wadau wengine wa maendeleo.
Naye dada wa familia ya watoto waliofaidika na mradi huo wa nyumba, Veronica, amesema upatikanaji wa nyumba hiyo umeleta faraja, usalama na matumaini mapya kwa familia yao baada ya muda mrefu kuishi katika mazingira yasiyokuwa rafiki.
Veronica amesema nyumba hiyo imewapa nafasi ya kuishi kwa amani na heshima, huku akieleza kuwa msaada huo una thamani kubwa kwa familia yao.
“Tunawashukuru sana Habitat for Humanity Tanzania kwa kutuwezesha kupata makazi bora na salama.
Msaada huu umeleta faraja, usalama na matumaini mapya katika maisha yetu. Kwa kweli, nyumba hii si makazi tu kwetu, bali ni zawadi yenye thamani kubwa ambayo imetupa nafasi ya kuishi kwa heshima na amani,” amesema Veronica.
Amesema familia yao inathamini mchango uliotolewa na Habitat for Humanity Tanzania pamoja na Serikali na wadau wengine waliohusika kuhakikisha nyumba hiyo inakamilika na kukabidhiwa kwa familia yao.
Veronica amewashukuru wadau hao kwa kujali familia zenye uhitaji na kuwataka kuendelea na moyo huo wa kusaidia wananchi wengine wanaokabiliwa na changamoto za makazi.
“Tunawashukuru kwa moyo wa upendo na kujali familia zenye uhitaji. Mungu awabariki sana kwa kubadilisha maisha yetu na kutupatia tumaini jipya,” amesema.
Makabidhiano ya nyumba hiyo yameongeza wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana na Serikali na Habitat for Humanity Tanzania katika kutafuta suluhisho la changamoto za makazi, hususan kwa familia zenye kipato cha chini na makundi yenye uhitaji.


Post a Comment