Na Given Kitunda, Mbeya.
Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, Patali Shida Patali, amewasisitiza wananchi wa Kata ya Itewe, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya, kusimamia na kulinda mradi wa ujenzi wa Daraja la Idunda, ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
Patali ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kumkabidhi mkandarasi eneo la ujenzi wa daraja hilo, akieleza kuwa mradi huo utasaidia kutatua changamoto za usafiri na mawasiliano zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo.
Amewataka wananchi kushirikiana na mkandarasi wakati wa utekelezaji wa mradi huo, pamoja na kuhakikisha miundombinu hiyo inalindwa mara baada ya kukamilika.
Kwa upande wake, Marko Gregory, mkandarasi wa mradi huo kutoka kampuni ya Kwaya Group, amesema anatarajia kuanza rasmi ujenzi wa daraja hilo Septemba 21, 2026, huku mkataba ukiwa na muda wa miezi sita.
Hata hivyo, mkandarasi huyo amesema anatarajia kukamilisha kazi hiyo ndani ya miezi mitatu, sawa na kufikia mwezi Desemba mwaka huu.
Nao baadhi ya wananchi wa Kata ya Itewe wameushukuru uongozi kwa kupeleka mradi huo, huku wakimuomba mkandarasi kuanza kazi kwa kasi na kuhakikisha daraja hilo linakamilika kwa wakati, ili kuwawezesha kuendelea na shughuli zao za kila siku bila changamoto ya usafiri na mawasiliano.


Post a Comment