Mwigulu: Tutengeneze mabilionea Watanzania kupitia madini


Na Mwadishi Wetu, Simiyu.

Serikali imetangaza mpango wa kuwawezesha vijana kuingia na kukua katika sekta ya madini, huku Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akitaka maeneo yenye leseni ambazo hazijaendelezwa yafunguliwe kwa vijana wenye nia ya uchimbaji.

Dkt. Mwigulu amesema lengo si kuongeza idadi ya wachimbaji wadogo pekee, bali kuwawezesha kukuza shughuli zao na hatimaye kujenga kampuni na biashara kubwa zinazomilikiwa na Watanzania.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha utajiri wa madini unazalisha fursa za kiuchumi kwa wananchi, hasa vijana ambao mara nyingi hukabiliwa na changamoto ya kupata maeneo rasmi ya kufanya shughuli za uchimbaji.

“Tunataka wachimbaji hawa wadogo nao wakue, tutengeneze mabilionea wa Kitanzania; ndiyo maana rasilimali hizi zililetwa hapa Tanzania ziwanufaishe Watanzania,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jumanne, Septemba 15, 2026, wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Sapiwi, Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu, alikokuwa katika ziara ya kikazi.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali imebaini changamoto ya baadhi ya watu kumiliki leseni nyingi za madini kwa muda mrefu bila kuendeleza maeneo hayo, hali inayowafanya vijana kushindwa kupata maeneo ya kufanya shughuli za uchimbaji.

Amesema hali hiyo haiendani na azma ya Serikali ya kuongeza ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini.

“Mtu mmoja anakuwa na leseni nyingi, ameshikilia miaka 10, vijana wanatafuta pa kuchimba... hili nimemwelekeza Waziri wa Madini afanye tathmini, aliye na leseni asiyoifanyia kazi, apewe vijana wapate pa kuchimba,” amesema.

Amemuagiza Waziri wa Madini kufanya tathmini ya leseni zinazoshikiliwa kwa muda mrefu bila kuendelezwa na kuchukua hatua kwa zile zitakazobainika kutotumika kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa.

Kwa mtazamo wa Serikali, hatua hiyo inalenga kuongeza matumizi ya maeneo yenye leseni na wakati huohuo kupanua nafasi kwa vijana kuingia katika shughuli rasmi za uchimbaji.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu pia alitoa maagizo kuhusu miundombinu, afya, mifugo, usimamizi wa vitendea kazi vya wananchi na sekta ya pamba.

Kuhusu barabara, alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kuhakikisha barabara ya Somanda–Nkololo–Matongo–Igegu inapandishwa hadhi kuwa ya Mkoa ili iweze kuhudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Alisema kabla ya mchakato huo kukamilika, ujenzi wa madaraja katika maeneo hatarishi unapaswa kupewa kipaumbele ili kupunguza usumbufu wa usafiri na vifo vinavyoweza kusababishwa na maji.

“Hii barabara pandisheni, iende ihudumiwe na TANROADS, ipandisheni kwenye hadhi ya mkoa ili ipate uamuzi wa mwisho lakini kabla ya hapo, madaraja lazima yajengwe, wananchi wasikwame na wakati huo huo tusiwe tunapoteza maisha ya watu kwa kusombwa na maji,” amesema.

Katika afya, Dkt. Mwigulu amekemea tabia ya wagonjwa wanaopewa rufaa kutozwa fedha za mafuta ya magari ya wagonjwa.



Amesema ambulance zinapaswa kuwa na mafuta na madereva wakati wote ili wagonjwa wanaohitaji huduma za rufaa waweze kupelekwa hospitalini kwa wakati.

 “Mgonjwa ameshapewa rufaa anatakiwa apelekwe hospitali ya rufaa, anatakiwa apelekwe kwa haraka. Ambulance ipo, mara zote ambulance iwe na mafuta na iwe na dereva,” amesema.

Ameagiza watumishi watakaobainika kuwatoza wagonjwa fedha kwa ajili ya mafuta kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Waziri Mkuu pia amesema Serikali imeondoa utaratibu wa kutaifisha mifugo ya wananchi, huku akisema sheria zinazohusiana na mifugo, wanyamapori na maeneo ya hifadhi zitaendelea kufanyiwa mapitio.

Aidha, amewaagiza viongozi na watendaji kuacha tabia ya kukamata vitendea kazi vya wananchi, ikiwemo pikipiki, bajaji, baiskeli na mikokoteni, pale ambapo makosa yanaweza kushughulikiwa kwa njia ya faini.

Katika kilimo, amemuagiza Waziri wa Kilimo kukutana na wadau wa pamba ndani ya mwezi mmoja na kuwasilisha mapendekezo ya mfumo bora wa ununuzi wa zao hilo.

Lengo, amesema, ni kuhakikisha mfumo huo unawanufaisha wakulima na kuchochea ongezeko la uzalishaji.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amesema Serikali imetumia zaidi ya Sh10 bilioni kutekeleza miradi 22 ya maji katika Jimbo la Bariadi Vijijini.

Amesema Sh3.2 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha miradi mitatu ya maji.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande, amesema Serikali imepokea madai 516 ya madhara yaliyosababishwa na wanyamapori katika mwaka wa fedha 2024/25 hadi 2025/26.

Kati ya madai hayo, amesema 469 yamelipwa huku yaliyobaki yakiendelea kushughulikiwa.

Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, Dkt. Festo John Dugange, amesema Serikali imetenga Sh40 milioni kwa ajili ya usanifu wa madaraja mawili ya Duma na Gambosi.

Amesema pia barabara ya Dutwa kuelekea Hospitali ya Wilaya tayari ina mkandarasi.



Post a Comment

Previous Post Next Post