Uongezaji wa virutubisho kwenye vyakula kulenga kupungzuza udumavu, upungufu wa damu



Na Wellu Mtaki, Tanga


WANANCHI wametakiwa kuzingatia matumizi ya vyakula vilivyoongezwa virutubishi muhimu mwilini, ikiwemo unga wa mahindi, mafuta ya kula na chumvi yenye madini joto, katika juhudi za kukabiliana na changamoto za lishe, ikiwemo udumavu kwa watoto, uzito pungufu na upungufu wa damu.

Hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa virutubishi muhimu kupitia vyakula vinavyotumiwa na wananchi katika maisha yao ya kila siku, huku wazalishaji wakihimizwa kuzingatia taratibu za uongezaji virutubishi ili kusaidia kuboresha afya ya jamii.

Akizungumza kuhusu juhudi hizo, Afisa lishe Mwandamizi Wizara ya Afya Peter kaja  alisema kuwa elimu inaendelea kutolewa kwa wazalishaji na wajasiriamali kuhusu umuhimu wa kuongeza virutubishi kwenye vyakula, pamoja na kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa miongozo inayohusika.

Alisema uongezaji virutubishi ni miongoni mwa njia zinazoweza kusaidia kupunguza matatizo ya lishe, hasa pale ambapo vyakula vinavyotumika mara kwa mara vinaongezewa virutubishi vinavyohitajika mwilini.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, mkoa wa Tanga una kiwango cha udumavu cha asilimia 24.1, huku uzito pungufu ukitajwa kuwa asilimia 11.2. Aidha, kiwango cha ukondefu kwa watoto kimetajwa kuwa asilimia 5.6, hali inayohitaji juhudi zaidi za kuboresha lishe na afya ya watoto.

Alieleza kuwa kipindi cha ujauzito hadi mtoto anapofikisha umri wa miaka miwili ni muhimu katika ukuaji na maendeleo yake, hivyo wazazi na walezi wanapaswa kuzingatia lishe bora kwa mama na mtoto katika kipindi hicho.

Katika hatua nyingine, alisema unga wa mahindi unaoongezwa virutubishi unaweza kusaidia kukabiliana na upungufu wa baadhi ya virutubishi mwilini, kutokana na matumizi yake kuwa sehemu ya chakula cha kila siku kwa kaya nyingi.

Alitaja baadhi ya virutubishi vinavyoweza kuongezwa kwenye unga huo kuwa ni madini ya chuma, zinki na vitamini mbalimbali, vinavyosaidia kukidhi mahitaji ya mwili na kuimarisha afya kulingana na mahitaji ya mtu.

Madini ya chuma ni muhimu katika utengenezaji wa hemoglobini inayosaidia kusafirisha oksijeni kwenye damu, huku zinki ikichangia ukuaji na utendaji wa kinga ya mwili.

Aliongeza kuwa elimu kuhusu lishe bora inapaswa kuzingatia pia mahitaji ya watoto wanaoanza kula vyakula vya nyongeza wanapofikisha umri wa miezi sita, kwa kuzingatia aina ya chakula, ubora wake na namna kinavyoandaliwa.

Kwa upande wa mafuta ya kula, alisema juhudi zinaendelea kuhamasisha uongezaji wa virutubishi vinavyohitajika, huku chumvi ikisisitizwa kuongezewa madini joto kwa mujibu wa viwango vinavyotakiwa.

Akizungumzia uzalishaji wa chumvi mkoani Tanga, alisema eneo hilo lina shughuli nyingi za uzalishaji wa chumvi, hivyo ni muhimu kuwawezesha wazalishaji ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinazingatia taratibu za uongezaji madini joto.

Alifafanua kuwa madini joto ni muhimu katika utendaji wa tezi ya thyroid na uzalishaji wa homoni zinazohusika na ukuaji na maendeleo ya mwili. Upungufu wake unaweza kusababisha matatizo ya kiafya, ikiwemo kuvimba kwa tezi hiyo, hali inayojulikana kama goita.

Alisisitiza kuwa uongezaji virutubishi kwenye vyakula unapaswa kwenda sambamba na elimu kwa wananchi, usimamizi wa wazalishaji na matumizi sahihi ya vyakula vyenye virutubishi, ili kuchangia kupunguza changamoto za lishe na kuboresha afya ya jamii.

Post a Comment

Previous Post Next Post